Masheikh wa Uasin Gishu Wadai Mageuzi Idara ya Usalama, Waonya Mambo Yanavyoelekea 2027
Viongozi wa Kiislamu Kaunti ya Uasin Gishu wameitaka serikali kufanya mageuzi makubwa katika Wizara ya Usalama wa Ndani na vyombo vyote vya usalama, wakisema vimeshindwa kuchukua hatua kali dhidi ya matamshi ya uchochezi na chuki ya kisiasa.
Wakizungumza Jumanne mjini Eldoret, viongozi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa CIPK Kanda ya North Rift Sheikh Abubakar Bini, pamoja na Mohammed Ali na Abdulkadir Mohammed, walisema hali ya kisiasa nchini inaelekea kwenye hatari kama hatua hazitachukuliwa mapema.
Sheikh Bini alisema kazi ya vyombo vya usalama ni kumlinda kila Mkenya bila kujali cheo au ushawishi wake kisiasa.
“Jukumu la vyombo vya usalama ni kuhakikisha kila Mkenya yuko salama. Sheria haipaswi kutumika kwa kuchagua watu. Inapaswa kutekelezwa kwa usawa, bila woga wala kuonea mtu,” alisema Bini.
Alionya kuwa taifa haliwezi kusubiri hadi chuki igeuke kuwa vurugu ndipo serikali iamke, na kusema dalili za hatari tayari zinaonekana kwenye mikutano ya kisiasa kote nchini kuelekea 2027.
“Hatuna budi kuchukua tahadhari sasa. Dalili zipo wazi. Tusipozuia uchochezi sasa, tutaishia kwenye machafuko,” alisema.
Mohammed Ali kwa upande wake alisema Wakenya wamechoshwa na namna mikutano ya kisiasa inavyosimamiwa, huku wengine wakiruhusiwa kusema chochote bila kuchukuliwa hatua.
“Tunataka taaluma na haki. Kila mtu ana haki ya kufanya siasa kwa amani bila kutishiwa, kupigwa au kutukanwa kikabila,” alisema.
Aliwataka wanasiasa kutumia majukwaa yao kuunganisha Wakenya badala ya kugawanya jamii kwa maneno yenye sumu.
Abdulkadir Mohammed alisema ni lazima sheria ifuate mkondo wake bila kuangalia mtu ni nani.
“Kwenye sheria hakuna mnyonge wala mkubwa. Kama umekosea, unapaswa kuitwa na kujibu maswali mbele ya vyombo halali, bila kujali kama wewe ni maarufu au una nguvu kisiasa,” alisema.
Viongozi hao wameitaka Tume ya NCIC na DCI kutokuwa na mchezo katika kushughulikia kesi za uchochezi na chuki, na badala yake zifanye kazi kwa uhuru bila kuingiliwa kisiasa.
Wametaja vurugu za hivi karibuni zilizoshuhudiwa Homa Bay kama mfano wa nini kinaweza kutokea kama vyombo vya usalama havitajiimarisha.
“Yaliyotokea Homa Bay yanapaswa kutufungua macho. Ni lazima tujipange sasa kabla mambo hayajaharibika zaidi,” aliongeza Bini.
Pia wamedai mabadiliko ya uongozi ndani ya Jeshi la Polisi, wakisema mabadiliko hayo yatarudisha imani ya wananchi kwa idara hiyo.
Walisema kudumisha amani ni jukumu la kila mtu — serikali, wanasiasa, viongozi wa dini na wananchi.
“Kenya ni yetu sisi sote. Lazima tuilinde kwa kuheshimu sheria na kuhakikisha inafanya kazi kwa kila mtu kwa usawa,” alihitimisha Mohammed Ali.
Viongozi hao walihitimisha kwa kuvitaka vyombo vya usalama kutenda kazi kwa weledi na kujitegemea, kwani uchochezi ukiachiwa utaathiri utulivu na mshikamano wa taifa kuelekea uchaguzi ujao.


