Uasin Gishu: Mashirika ya Kutetea Haki Yamlalamikia OCS wa Eldoret Central, Yataka IGP Aingilie Kati - News Light Kenya

Uasin Gishu: Mashirika ya Kutetea Haki Yamlalamikia OCS wa Eldoret Central, Yataka IGP Aingilie Kati

Hali ya joto imezidi kuongezeka katika sekta ya usalama Kaunti ya Uasin Gishu baada ya mashirika ya kutetea haki za binadamu kudai uchunguzi wa haraka na wa kujitegemea dhidi ya Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Eldoret Central, Chief Inspector James Lenaso.

Mashirika hayo yakiongozwa na Mkurugenzi wa Centre Against Torture, Kimutai Kirui na Juma Akumu kutoka Eldoret Social Justice Centre, yametangaza kuwa tayari yamepeleka malalamiko yao kwa Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, yakimtaka aagize uchunguzi kubaini ukweli wa madai yanayomzunguka OCS huyo.

Kulingana na barua yao ya malalamiko, Lenaso anakabiliwa na tuhuma tatu kuu. Kwanza, anatuhumiwa kutumia vibaya madaraka yake ya kipolisi. Pili, anatuhumiwa kuchapisha hadharani majina na picha za watu wanaoshukiwa kutenda makosa kwenye mitandao ya kijamii kabla hata hawajafikishwa mahakamani. Tatu, kuna madai kuwa baadhi ya washukiwa wamekuwa wakiombwa pesa ili kuachiliwa.

“Hatua ya kupiga picha washukiwa na kuzisambaza mtandaoni ni kinyume na sheria na ni aibu kubwa. Sheria inasema mtu hana hatia mpaka mahakama iamue. Hii ni ukiukaji wa haki za binadamu,” alisema Kirui.

Kirui aliongeza kuwa kitendo hicho hakidhalilishi tu washukiwa, bali pia kinaweza kuharibu kesi mahakamani kwa kuwa jamii inawaona kama wahalifu kabla ya kesi kusikilizwa.

Juma Akumu alisema wamelazimika kuandika kwa IGP baada ya kupokea malalamiko kadhaa kutoka kwa wakazi wa Eldoret wanaodai wameombwa hela kituoni hapo.

“Watu wamekuja kwetu wakilalamika. Wengine wanasema waliombwa pesa ili ndugu zao waachiliwe kwa dhamana ya polisi ambayo kisheria ni bure. Tunataka ukweli ujulikane. Kama ni kweli, basi ni ufisadi unaofanyika ndani ya kituo kikuu cha polisi mjini Eldoret,” alisema Akumu.

Watetezi hao wamesisitiza kuwa ombi lao ni kuhakikisha uchunguzi unafanywa kwa haki na uwazi, na si kumhukumu OCS kabla ya ukweli kujulikana. Wamesema wanataka kubaini iwapo taratibu za polisi zilifuatwa kama inavyotakiwa na sheria.

“Tunachotaka ni uchunguzi huru. Tujue kama madaraka yalitumiwa sawasawa. Kama hakuna makosa, basi afisa atasafishwa jina lake. Lakini kama kuna makosa, hatua zichukuliwe,” walisema.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Uasin Gishu, Wilberforce Shicharani, alisema bado hakuwa amepata malalamiko hayo rasmi wakati alipotafutwa na wanahabari, hivyo hakuwa tayari kuyajibu kwa kina.

Alisema hata hivyo, Jeshi la Polisi lina utaratibu wa ndani wa kushughulikia malalamiko dhidi ya maafisa wake na kwamba malalamiko yoyote yatakayowasilishwa yatachunguzwa.

Hadi sasa, tuhuma dhidi ya Chief Inspector James Lenaso bado ni madai ambayo hayajathibitishwa na vyombo huru vya uchunguzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *