“Goons ” Walinzi Wapya Wa Wanasiasa Kenya

Binadamu akishakula chakula ashibe, apate pesa atajirike, ashike hatamu ya uongozi alewe na mamlaka, hakika huwa na uhuru uliopitiliza wa kufanya jambo lolote lile ikiwemo kujiundia sheria, sio sheria tu, sheria zinazomnufaisha yeye binafsi na watu wake wa karibu, hujiongezea mamlaka, hufanya maamuzi ya kustaajabisha Kutokana na shibe na nishai aliyo nayo.
Katika siasa za Kenya, haswa karne ya 21, zimechukua mkondo mwingine. Sio tena siasa za nipe nikupe bali zimegeuka kuwa siasa za nipate nikupate, nikosoe ukione!

Wanasiasa wengi sasa hivi wanajilinda na kulinda maslahi pamoja na kuwazima wapinzani wao wanaowakosoa au wale wanaoenda kinyume na matakwa yao, kwa kutumia wahuni “goons” ili kuwazima na kuwatokomeza.

Wahuni hawa wamekuwa kama ndio walinzi nambari wani wa wanasiasa hata kuliko polisi, washika doria halali.
Kwanini? Kaa kitako nikudadavulie kwa kina bila wahaka wowote. Wahuni hawa huwa hawazingatii wala kufuata sheria iliyoko kwenye katiba, kwa hivyo wana uhuru chungu nzima wakutekeleza uovu wowote ule kulingana na maagizo ya “mwajiri” wao.

Pili, wao huwa wameficha nyuso zao au utambulisho mara nyingi, kwa maana hiyo, waneza wakatekeleza shughuli za kinyama bila kujulikana na umma au dola za kiusalama.

Malipo yao huwa ni nafuu ukilinganisha na yale ya polisi, sasa hapa wanasiasa hufadhalisha wawatumie hawa wahuni kwa shughuli zao bila ya kutoboka mifuko yao sana.

Kwa wanasiasa wenyewe hujiona wamejiongezea ulinzi maradufu huku wakiwa na matumaini ya kwamba wataogopewa sana na wananchi na wapinzani wao.

Lakini la kustaajabisha ni kwamba, wanasiasa wenzao pia wamo mbioni kuwasajili na kuwakodi wahuni hao kwa male go na nia ile ile kama yao.
Tumewasikia baadhi ya viongozi wakilalama kuhusu baadhi ya wanasiasa kutumia wahuni kuvamia mikutano na wanasiasa wengine.

Wale wale viongozi wanaolia mbele ya umma ndio pia wanamiliki wahuni pia.
Ama ndiyo ile ajira waliyoahidi vijana nchini? Inasikitisha sana.

Sasa hapa ni pa mwenye Nguvu mpishe! Haijalishi yuko serikalini au upinzani nguvu ya wahuni wake ndio kusema.
Siasa za Kenya zinaelekea wepi? Ama kweli fisi aliyeshiba haulizwi alichokula!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *